NAIBU KATIBU MKUU OR-TAMISEMI (ELIMU) AFANYA ZIARA MANISPAA YA KIGAMBONI,MPANGO UBORESHAJI MIUNDOMBINU SHULE ZA MSINGI WAPAMBA MOTO
Leo hii 16/11/2022 Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI (elimu)ndg.Ramadhani Kailima amefanya ziara katika Manispaa ya Kigamboni kwa nia ya kukagua miradi pamoja na kutembelea shule za msingi zenye changamoto za miundo mbinu.
Akiwa katika ziara hii Ndg.Kailima amepitia shule takribani tano na kufanya ukaguzi wa miundo mbinu inayohitaji ukarabati na mapungufu upande wa madawati,matundu ya vyoo,ofisi za walimu.Shule zilizotembelewa ni AboudJumbe,Kidete,Kibugumo, Mjimwema na Kisota.
Aidha katika ziara hiyo ndg.Kailima amejionea uchakavu wa madarasa mbalimbali yanayohitaji kukarabatiwa,upungufu matundu ya vyoo,upungufu wa madawati na madarasa na kujazana kwa wanafunzi katika madarasa kutokana na kutotosheleza.
Akizungumza amesema mapungufu yote aliyoyashuhudia ameyachukua kwa ajili ya kwenda kuyawasilisha ili yafanyiwe kazi kupitia Mpango huu wa serikali ya awamu ya sita ambapo sasa inaenda kuboresha miundo mbinu ya shule za msingi kama ilivyofanya kwa shule za sekondari.
"Tunamshukuru Mh.Rais wetu kwa kuja na mpango huu ambao sasa unaenda kutatua changamoto kwa upande wa shule za Msingi."alisema ndg.Kailima
Pamoja na ukaguzi wa miundo mbinu Naibu Katibu Mkuu amekagua pia baadhi ya madarasa ya kidato cha kwanza yanayojengwa hivi sasa kupitia fedha za kapu la mama ambapo kwa Manispaa ya Kigamboni ilipata shs.Mil.200 kutekeleza ujenzi wa madarasa 10.
Pamoja na hayo amegusia suala la udhalilishaji wa watoto kushika kasi hivyo amewataka walimu kuwa karibu na wanafunzi ili kuyajua wanayopitia kwa upande huo na ameshauri kuwepo kwa Dawati linaloshughulika na maswala ya udhalilishaji wa wanafunzi.Pia suala la madawa ya kulevya halikuwa nyuma kwani amewataka walimu kuwa makini na wauzaji wa biskuti na pipi wanaofika mashuleni kuuzia watoto kwani umezuka mtindo wa kuweka madawa ya kulevya katika pipi na biskuti jambo linalopelekea watoto kujiingiza katika madawa ya kulevya bila kujijua.
Ziara hii ni kufuatia mpango huo wa uboreshaji wa miundombinu kwa shule za msingi ambao serikali ya awamu ya sita ya Mh.Samia Suluhu Hassan imeamua kuutekeleza ili kuboresha miundo mbinu ya shule za msingi,hivyo unafanyika ukaguzi katika mashule kubaini maeneo yote yanayohitaji kuboreshwa, aidha ni utekelezaji wa Ilani ya chama cha Mapinduzi katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Imetolewa na kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
Gezaulole Kata ya Somangila, Kigamboni
Anuani ya Posta: 36009 Dar es Salaam
Simu: +255222928468
Simu ya Mkononi: +255222928468
Bara pepe: info@kigambonimc.go.tz
Haki MilikiĀ©2017 Manispaa ya Kigamboni . Haki zote Zimehifadhiwa