Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni Arch.Ngwilabuzu Ludigija leo amekabidhiwa rasmi zahanati ya Mtaa wa Kijaka iliyopo kwenye Kata ya Kimbiji ambayo imejengwa kwa ushirika wa Shirika lisilo la Serikali Caritas Jimbo kuu Katoliki la Dar es Salaam ambao wamekamilisha ujenzi wa jengo hilo kwa gaharama za Milioni 69.46 huku nguvu za wananchi ikiwa ni milioni 7.6 na Mfuko wa jimbo Milioni2.
Akipokea makabidhiano hayo kwenye Zahanati hiyo kutoka kwa Mkurugenzi wa Caritas Jimbo la Dar es Salaam, Mkurugenzi amesema kwamba anashukuru sana kwa msaada amabao Caritas wameutoa kwa wananchi wa Kijaka ambao utarahisisha upatikanaji wa huduma kwao ambapo utapunguza vifo vya mama na mtoto.
Mkurugenzi amesema kuwa Kigamboni ni Manispaa changa na inaupungufu mkubwa wa miundombinu kwenye sekta za elimu, zahanati kila mitaa, ofisi za watendaji wa Kata na Mitaa hivyo kama Serikali wanalazimika kushirikiana na wadau wa maendeleo kama caritus kutatua baadhi ya changamoto hivyo anawaomba caritus kuendelea kuisapoti Manispaa.
Aidha amewataka wananchi waliokabidhiwa Zahanati hiyo kuhakikisha wanaitunza kwa kupanda miti na maua ambayo yatafanyika kama kivuli na mapumziko kwa wagonjwa watakaofika kuhudumiwa hapo, na kuwaomba kutoa ushirikiano kwa wahudumu walioletwa kwenye Zahanati hiyo.
Mkurugenzi amewapongeza wananchi wa Kijaka kwa Umoja na nguvu kazi walizojitolea kufikisha jengo hilo kwenye hatua ya lenta na kuwaomba viongozi wa Kimbiji kuhamasisha wananchi kujitolea nguvu kazi ili wafadhili na Serikali wanapoombwa kuwasaidia iwe rahisi tofauti na kama wananchi wanapoomba msaada wakiwa hawajaaanza kufanya kitu chochote.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya kigamboni Dkt.Charles Mkombachepa ameshukuru uongozi wa Caritus kwa kuwasogezea wananchi wa Kijaka huduma Karibu na kusema kuwa zahanati hiyo inafanya jumla ya zahanati 20 zinazomilikiwa na Serikali na inatarajiwa kuhudumia wananchi zaidi ya 500 ambapo tangu mei ilipoanza kufanya kazi imehudumia wagonjwa 176.
Mganga Mkuu amesema kuwa Caritus wanaisaidia Kigamboni kuendana na kasi ya Rais na utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya kusogeza na kuimarisha huduma za afya kwa wananchi hususani wale waliopo pembezoni mwa mji ambao wanapata changamoto kuzifata huduma maeneo ya mbali .
Mkurugenzi wa Caritus Jimbo kuu la Dar es salaam Christian amesema kuwa fedha zilizotolewa zimesaidia kurekebisha kuta za jengo na kuweka madirisha ya vioo,kuweka dari(gypsum), kupiga plasta na rangi,kupiga bati la paa rangi, kuchimba kisima,tanki la maji, umeme wa jua(solar),ufungaji wa solar kwaajili ya kupampu maji pamoja na mtandao wa taa kwenye maeneo yanayozunguka Zahanati.
Ameongeza kuwa fedha pia zimetumika kujenga vyoo,ujenzi wa sehemu maalumu ya kuchomea taka,feni zinazotumia solar na televisheni itakayowawezesha wagonjwa kupata elimu ya afya na namna bora ya kujikinga na maradhi mbalimbali.
Aidha ameshukuru uongozi wa kijaka kwa kujali afya ya jamii na kuanzisha mradi huo na kusema kuwa hiyo ndiyo tafsiri mojawapo sahihi ya maendeleo ya jamii inayosisitizwa na Serikali hivyo wataendelea kuunga mkono juhudi za Serikali.
Diwani wa Kata ya Kimbiji Mhe. Sanya Bunaya ameshukuru Caritus na Mkurugenzi kwa namna ya Kipekee walivyowasaidia wakazi wa Kijaka kupata huduma za afya na kwamba yeye kama kiongozi atahakikisha kuwa kipaumbele katika kuwahamasisha wananchi kujenga mazoea ya kujitolea nguvu kazi zao ili kujiletea maendeleo yao wenyewe.
Zahanati ya Kijaka ilianza ujenzi rasmi mwaka 2008 kupitia nguvu za wananchi baada ya kuona uhitaji mkubwa wa huduma za afya ambapo baada ya Caritus kupokea maombi ya ukamilishwaji wa jengo hilo Januari 2019, Aprili 2019 waliwezesha kumalisha jengo hilo na huduma kuanza kutolewa rasmi mei 2019.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni Arch.Ng'wilabuzu Ludigija akipokea feni kutoka kwa Mkurugenzi wa Caritus Jimbo kuu la Dar es Saam kwaajili ya watumishi wa Zahanati hiyo
Baadhi ya wananchi wa Kijaka waliofika kushuhudia makabidhiano hayo
Mkurugenzi wa Caritus akionesha cheti cha shukurani alichopokea kutoka kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni
Stoo ya dawa
Chumba cha Kujifungulia/uzazi
Jengo la Maliwato
Wananchi wa Kijaka wakiimba ngonjera ya shukurani kwa kupatiwa Zahanati hiyo.
Muonekano wa jengo la Zahanati kwa mbele
Mganga mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Dkt.Charles Mkombachepa akizungumza na wananchi na kutoa shukurani
Gezaulole Kata ya Somangila, Kigamboni
Anuani ya Posta: 36009 Dar es Salaam
Simu: +255222928468
Simu ya Mkononi: +255222928468
Bara pepe: info@kigambonimc.go.tz
Haki MilikiĀ©2017 Manispaa ya Kigamboni . Haki zote Zimehifadhiwa