Manispaa ya kigamboni imetoa jumla ya Tsh. Mil 996.4 Mkopo wa asilimia 10
Mkuu wa Wilaya Kigamboni Mh. Bulembo amewataka wanufaika wa mkopo wa asilimia 10 unaotokana na mapato ya ndani kuzitumia fedha hizo kwa malengo kusudiwa ambao wameuanisha katika maombi ya mkopo waliowezeshwa.
Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji wa mikopo iliyofanyika leo Machi 22,2023 katika viwanja vya ofisi ya manispaa kigamboni Katibu Tawala bi Pendo Mahalu aliyemuwakilisha Mkuu wa Wilaya ametumia nafasi hiyo kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji kwa jitihada zake za dhati za usimamizi wa sheria inayowataka kutenga asilimia kumi ya fedha zinazotokana na mapato ya ndani na kuzitoa kwa makundi nufaika ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kwa mikopo isiyo na riba na yenye masharti nafuu.
‘Nikupongeze Mkurugenzi na wataalam wote ndani ya Manispaa hii kwa kuendelea kutenga fedha na kuzitoa kwa makundi kusudiwa, kitendo mkifanyacho ni cha kiungwana na mmekua sehemu ya kupiga vita umasikini kwa wananchi wa Manispaa hii’ alisema.
Veronica Kiluvia Afisa maendeleo ya Jamii aliyemuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji alisema ni fahari kwao kuona wamekua sehemu ya kuinua maisha ya wananchi wanaoishi kigamboni.
‘ Leo mmeweza kupatiwa fedha, mmewezeshwa kwenda kutimiza malengo mliyojiwekea kama kikundi niwaombe mkazitumie fedha hizi vizuri na mrejeshe kwa wakati ili kila mwananchi anayeishi ndani ya halmashauri hii iweze kumsaidia kupitia mikopo isiyo na riba na yenye masharti nafuu.
Akiendelea Bi kiluvia alibainisha pamoja na kuwepo kwa mafanikio zipo changamoto zinazosababishwa na wachache ambao wamekua wagumu kurejesha mikopo hiyo inayopelea kukwamisha wengine kuipata mikopo kwa wakati stahiki.
Aidha wanufaika wa mkopo bi Vaileth Rweyemamu na Amiri Kawale wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kupata mkopo na wameahidi kuirejesha kwa wakati ili kuwezesha wananchi wengine kunufaika.
Manispaa ya kigamboni imetoa jumla ya Tsh. Mil 996.4 ikiwa ni fedha ya asilimia 10 mapato ya ndani kwa robo ya kwanza na ya pili kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Gezaulole Kata ya Somangila, Kigamboni
Anuani ya Posta: 36009 Dar es Salaam
Simu: +255222928468
Simu ya Mkononi: +255222928468
Bara pepe: info@kigambonimc.go.tz
Haki Miliki©2017 Manispaa ya Kigamboni . Haki zote Zimehifadhiwa