Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 11 Februari, 2020 amezindua Wilaya ya Kigamboni Mkoani Dar es Salaam na pia amezindua jengo jipya la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo na jengo jipya la Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni.
Wilaya ya Kigamboni yenye eneo la kilometa za mraba 577.9 (hekta 57,786. ilianzishwa kwa tangazo la Serikali namba 462 la mwaka 2015 ikimegwa kutoka Wilaya ya Temeke kwa lengo la kusogeza karibu huduma kwa wananchi.
Mhe. Rais Magufuli amezindua jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni lenye ukubwa wa meta za mraba 1,285, lina uwezo wa kuchukua watumishi 50 na ujenzi wake umegharimu shilingi Bilioni 1.6.
Pia, Mhe. Rais Magufuli amezindua jengo la Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni lenye ukubwa wa meta za mraba 7,342, lina uwezo wa kuchukua watumishi 450 na ujenzi wake umegharimu shilingi Bilioni 5.2.
Katika hotuba yake, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Kigamboni kwa kusogezewa huduma za utawala na pia amewapongeza viongozi wa Kigamboni wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Sara Msafiri na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kujenga majengo hayo vizuri.
Mhe. Rais Magufuli ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha wilaya hii kwa kuhakikisha miundombinu inaimarishwa ambapo ametoa wiki 1 kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kukabidhi eneo lote la ekari 719 (lililokuwa likimilikiwa na Shirika la Taifa la Kilimo na Chakula - NAFCO) kwa Wilaya ya Kigamboni ili wilaya hiyo iliendeleze kwa kujenga majengo ya umma zikiwemo nyumba za watumishi.
Kuhusu changamoto ya barabara, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kushangazwa kwake na kitendo cha viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kutotenga fedha za kuboresha barabara za Kigamboni chini ya Mradi wa Maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP), hivyo ameagiza fedha za mfuko wa barabara zilizotengwa kwa ajili ya wilaya zilizonufaika na mradi wa DMDP zipelekwe Kigamboni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara ya lami ya mzunguko ya Kimbiji – Mjimwema.
Amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenister Mhagama na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Bw. William Erio kuchukua hatua dhidi ya mkandarasi aliyepewa zabuni ya kujenga kipande cha barabara cha kuunganisha na Daraja la Nyerere (Kigamboni) kutokana na mkandarasi huyo kupanga gharama kubwa za ujenzi kupita kiasi.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametoa wiki 1 kwa watumishi wa Wilaya ya Kigamboni hasa wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama kuhamia Kigamboni ikiwemo kuhamia katika majengo ya NSSF ambayo hayakaliwi na watu, badala ya kuishi katika wilaya zingine za Mkoa wa Dar es Salaam na pia ameiagiza TAMISEMI kutoa shilingi Bilioni 2 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa nyumba za watumishi katika eneo la Serikali lilitolewa kwa Manispaa hiyo kutoka NAFCO.
Mhe. Rais Magufuli amezungumzia mvua zinazoendelea kunyesha kwa kuwatahadhalisha Watanzania kutojenga makazi katika maeneo ya mabondeni na badala yake watumie mabonde na maji ya mvua zinazonyesha kwa kilimo badala ya kubaki wakilalamika.
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Magufuli akisaini kitabu cha wageni kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mhe. Sara Msafiri.
Raisi wa Tanzania Dkt. John Magufuli akisalimia vingozi mara baada ya Kigamboni
Rais wa Tanzania Dkt.John Magufuli akiwa amembatana na viongozi wengine wa Serikali kuelekea eneo la hafla ya uzinduzi wa Wilaya
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mhe. Sara Msafiri akifafanua jamboa kwa Raisi Dkt. John Magufuli walipofika kwenye jengo la Mkurugenzi.
Mkurugenzi wa Mnispaa ya Kigamboni Ng'wilabuzu Ludigija akifafanua jambo kwa Raisi wa Tanzania Dkt.John Magufuli alipotembelea jengo la Mkurugenzi.
Picha ya pamoja ya Raisi Dkt John Magufuli na viongozi wengine mara baada ya uzinduzi.
Jengo la Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni
Jengo la Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni
Gezaulole Kata ya Somangila, Kigamboni
Anuani ya Posta: 36009 Dar es Salaam
Simu: +255222928468
Simu ya Mkononi: +255222928468
Bara pepe: info@kigambonimc.go.tz
Haki Miliki©2017 Manispaa ya Kigamboni . Haki zote Zimehifadhiwa