Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mhe. Sara Msafiri amesema kuwa ameridhika na hali ya uendeshwaji wa kivuko hususani katika eneo la usalama baada ya kutoa maelekezo kwa wasimamizi wa kivuko kuboresha huduma zinazotolewa hapo.
Mhe. Sara amesema hayo leo alipofanya ziara ya ukaguzi wa utekelazaji wa maagizo aliyoyatoa alipotembelea kivuko hicho mwezi uliopita na kusema kuwa kwa kiwango kikubwa maelekezo yamefanyiwa kazi na mabadiliko makubwa yameonekana.
Aliongeza kuwa wametoa namba za simu za dharula kama alivyoelekeza, namba ya zimamoto na ukoaji, matangazo yanatolewa yanayoeleza utaratibu mzima wa kupata huduma za vivuko ikiwemo na uwezo wa vivuko ya ubebaji wa watu na magari, wamefunga luninga kwenye vivuko zinazoonesha video fupifupi za elimu ya uokoaji na mawasiliano kwa watumia vivuko.
“ walau sasa kuna elimu kidogo ya uokozi namna ya kutumia life jacket(vazi la uokoaji), maboya, namna ya kuruka kwenye maji, vifaa vimesafishwa na vimewekwa maeneo ya wazi hakuna kufuli kama zamani kwahiyo likitokea jambo lolote inakuwa rahisi kwa abiria kuvipata kwa haraka, kwa kiasi Fulani nimeridhika bado vitu vichache tu” Amesema Mhe. Sara
Aidha ameelekeza kufungwa kwa luninga kubwa kwenye maeneo ya kusubiria abiria ili elimu inayotolewa iweze kufikiwa na watumiaji wote wa vivuko,kuweka namba ya simu itakayopigwa bure na mwananchi ikiwa ni pamoja na kufunga kamera itakayosaidia kufuatilia mwenendo mzima wa huduma zinazotolewa na kivuko.
Akizungumzia suala la wavuvi amesema kuwa ni mtambuka kwasababu jinsi soko lilivyojengwa limelenga wafanyabiashara ambao ni wavuvi, mitumbwi iliyopaki pembezoni ambayo inaingilia njia za meli na vivuko lazima wadau wote wahusike kukaa kwa pamoja na kamati ya ulinzi na usalama kwasababu hawa wadau wanasheria zinazowaongoza kwa hiyo ni vyema utaratibu ukafuatwa katika kutatua changamoto hiyo.
Mkuu wa Wilaya pia amepiga marufuku mitumbwi kutumika kuvushia abiria kinyume na taratibu na kusema kwamba sheria zifuatwe kwa yeyote atakayebainika anatumia mitumbwi kuvusha abiria.
Kwa upande wake kaimu mtendaji mkuu wa TEMESA Eng.Japhet Masele ameshukuru na kusema kuwa maagizo mengi ambayo yalikuwa yametolewa yalikuwa yameanza kufanyiwa kazi katika kuboresha huduma za vivuko na kusema kuwa wamejipanga kuwa na usismamizi mkali kipindi cha asubuhi na jioni ambapo kunakuwa na abiria wengi na kueleza kuwa wanahakikisha vivuko vyote nchini vinafanya kazi kwa kuzingatia taratibu na kanuni.
Ameongeza kuwa hivi karibuni wanaweka mfumo wa kuhesabu(electronic counter) ili kivuko kinavyopakia uongozi uweze kujua kivuko kimeondoka na ujazo sawa kuepuka kuzidisha uwezo wa kivuko husika.
Mkuu wa Wilaya Mhe. Sara Msafiri akieleza namna alivyoridhishwa na maboresho ya huduma zinazotolewa na vivuko.
baadhi ya abiria wakishuka kwenyhe kivuko baada ya kufika ng'ambo
Mtoa elimu ya kujiokoa kwa kutumia vazi la uokoaji(life jacket) akitoa maelezo ya namna ya kulitumia vazi hilo
elimu ya kutumia boya ikitolewa na mkufunzi wa masuala ya ukoaji
Mkuu wa Wilaya akiwa ameambatana na viongozi wengine wakitoka kwenye kivuko cha Mv Magogoni
Kiongozi wa TEMESA aliyenyoosha mkono akieleza changamoto ya mitumbwi ya wavuvi
moja ya luninga iliyofungwa kwenye kivuko cha Mv Magogoni ikionesha video fupifupi za jinsi ya kujiokoa.
Gezaulole Kata ya Somangila, Kigamboni
Anuani ya Posta: 36009 Dar es Salaam
Simu: +255222928468
Simu ya Mkononi: +255222928468
Bara pepe: info@kigambonimc.go.tz
Haki Miliki©2017 Manispaa ya Kigamboni . Haki zote Zimehifadhiwa