*MTAKUWA Kigamboni waandaa Mkakati ulinzi mwanamke na Mtoto*
Kamati ya ulinzi na usalama wa mwanamke na mtoto Wilaya ya Kigamboni leo Desemba 7, 2022 imeketi na kuweka maazimio wanayotarajia kuyatekeleza ifikapo january 2023 huku wakipanga kujipima ifikapo mwezi Machi 2023.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Afisa Ustawi kiongozi wa Manispaa ya Kigamboni Bi. Sereti Kiroya alisema kuwa kamati hiyo haina budi kuweka mpango mkakati na kuanza kuutekeleza mapema Januari 2023 huku wakiweka mapendekezo ya kujipima ifikapo machi 2023 kwenye vikao vya robo ya tatu.
“Sisi kama kamati tumejiwekea mipango nane ambayo kimsingi inatupasa kuitumia kama sehemu ya majukumu yetu huku tukitumia mipango hiyo kama chombo cha kupima utendaji wetu wa ukamilifu wa yale tuliyojipangia,” alisema Bi Kiroya.
Aliitaja mipango waliyojiwekea kuwa ni pamoja na kukutana na kamati za ulinzi ngazi ya kata kwa lengo la kuwapa elimu watakayoitumia kufikisha kwa jamii, kuunda vikundi vya malezi kwenye maeneo ambayo havipo na kuvisimamia vile vilivyopo ili viweze kufanya kazi tarajiwa.
Naye Afisa Elimu vijana katika Manispaa hiyo Grace Muya alitoa pendekezo lake kwa kuitaka Kamati itoe elimu mashuleni hasa nyakati ambazo vikao vya wazazi na walimu vinafanyika kwani takwimu zinaonesha kuwa ukatili mkubwa wa kijinsia unaanzia ngazi ya familia.
KIkao hicho cha kamati ya ulinzi wa mwanamke na watoto kimehudhuriwa na wajumbe kutoka idara mbali mbali ikiwa na lengo la kuendeleza mpango mkakati wa Taifa wa kutokomeza ukatili wa wanawake na watoto (MTAKUWA).
Imetolewa na kitengo cha Mawasiliano Serikalini KGMC
Gezaulole Kata ya Somangila, Kigamboni
Anuani ya Posta: 36009 Dar es Salaam
Simu: +255222928468
Simu ya Mkononi: +255222928468
Bara pepe: info@kigambonimc.go.tz
Haki Miliki©2017 Manispaa ya Kigamboni . Haki zote Zimehifadhiwa