Mwenyekiti wa kamati ya Lishe Wilaya, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Mhe. Halima Bulembo, amewahimiza wataalamu wa afya ngazi ya wilaya na kata kuendelea kutoa elimu kuhusu lishe bora ili kupunguza changamoto zinazosababishwa na lishe duni.
Akizungumza leo katika kikao cha tathmini ya hali ya lishe kwa robo ya kwanza (Julai-Septemba 2024), Mhe. Bulembo alisisitiza umuhimu wa kutoa elimu ya lishe kwa jamii na kuchukua hatua za kuboresha hali ya lishe wilayani Kigamboni.
Aidha, aliwataka wataalamu wa kilimo kuongeza juhudi za kuhakikisha shule zote za msingi na sekondari zinaanzisha na kuendeleza bustani za mboga mboga zitakazosaidia kuboresha mlo wa wanafunzi.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya alibainisha kuwa Manispaa ya Kigamboni kupitia Idara ya Afya imeendelea kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa wanawake waliofikia umri wa kuzaa ili kukabiliana na changamoto za watoto kuzaliwa na uzito mdogo, na changamoto inayotokana na lishe duni wakati wa ujauzito.
Katika kikao hicho, wajumbe walipendekeza mikakati mbalimbali ikiwemo kuendelea kutoa elimu ya lishe kwa jamii kupitia mikutano ya mitaa na kushirikiana na Idara ya Kilimo ili kuwezesha kuanzishwa kwa bustani za mboga mboga katika ngazi za kaya na taasisi za elimu.
Mkutano huo unalenga kuimarisha jitihada za serikali katika kuhakikisha hali ya lishe bora kwa wananchi wa Kigamboni inaboreshwa kwa kiwango kikubwa.
Gezaulole Kata ya Somangila, Kigamboni
Anuani ya Posta: 36009 Dar es Salaam
Simu: +255222928468
Simu ya Mkononi: +255222928468
Bara pepe: info@kigambonimc.go.tz
Haki MilikiĀ©2017 Manispaa ya Kigamboni . Haki zote Zimehifadhiwa