BILIONI 1,225,251,681.56 KUNUFAISHA SEKTA YA ELIMU SEKONDARI KWA MWAKA WA FEDHA 2022/2023
Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1,225,251,681.56 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwa lengo la kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya elimu upande wa sekondari.
Fedha hizo zitaenda kutekeleza miradi mbalimbali ambayo NI ukamilishaji wa ujenzi wa majengo ya Utawala,ujenzi wa shule mpya ya sekondari,ununuzi wa madawati,ukarabati wa madarasa kwa yale yanayohitaji ukarabati na umaliziaji wa miundombinu.
Kwa upande wa ukamilishaji wa ujenzi wa majengo ya Utawala kata ya Kisarawe II Shule ya sekondari Kisarawe II na shule ya sekondari Nguva watanufaika kwa kukamilishiwa majengo hayo ambapo kwa kiasi kikubwa itatatua kero ya waalimu kukosa sehemu Sahihi na yenye usalama katika utekelezaji wa shughuli zao wawapo shuleni .
Aidha utafanyika ukamilishaji wa miundo mbinu katika shule ya sekondari Paul Makonda.
Ili kutatua kero za kubanana kwa wanafunzi Manispaa pia imepanga kutumia fedha hizo kwa ajili ya ununuzi wa madawati 600 kwa shule za sekondari.
Pamoja na hayo ili kutekeleza takwa la kiafya Manispaa kwa mwaka huu wa fedha itaboresha mazingira ya vyoo kwa kujenga matundu 5 ya vyoo vya waalimu katika shule ya sekondari Kibada na matundu 5 katika shule ya sekondari Mizimbini.
Elimu ya sayansi na teknolojia imeshika Kasi katika Karne hii ili kuendana na Kasi hii Manispaa imeamua kuhakikisha inafanya ukamilishaji wa maabara katika Kata zote ili Kurahisisha masomo haya ya sayansi kufundishwa kwa vitendo na kuleta ufanisi zaidi.
Jumla ya madarasa 32 yatafanyiwa ukarabati ambapo kwa kila shule yatakarabatiwa madarasa 4 ,shule hizo ni Tungi,Minazini,Vijibweni, Pembamnazi,Kisarawe II,Aboud Kumbe,Nguva na Kidete.
Aidha fedha hizo pia zitatumika kujenga shule mpya ya sekondari ya Mkoa itakayokuwa katika Kata ya Somangila.
Aidha umaliziaji wa ujenzi wa Maktaba,chumba cha ICT na vyoo vya walimu katika shule Shikizi Tundwi Songani iliyojengwa kutokana na mradi wa SEQUIP.
Fedha hizo zilizotengwa ni kwa chanzo cha Mapato ya ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni.
Imetolewa na kitengo cha Mawasiliano Serikalini KGMC
Gezaulole Kata ya Somangila, Kigamboni
Anuani ya Posta: 36009 Dar es Salaam
Simu: +255222928468
Simu ya Mkononi: +255222928468
Bara pepe: info@kigambonimc.go.tz
Haki MilikiĀ©2017 Manispaa ya Kigamboni . Haki zote Zimehifadhiwa