Wafanya biashara wa Chakula (Mama na Baba Lishe) kata ya Pemba mnazi Leo Septemba 25,2023 wamemshukuru na kumpongeza Mkuu wa wilaya ya Kigamboni Mhe. Halima Bulembo kwa kutenga mda na kufanya ziara ya kuwatembelea kwenye maeneo yao ya biashara huku akipokea changamoto zinazowakabili na kuzitatua.
Akiwasilisha shukrani hizo kwa niaba ya baba na mama lishe Shabani Mwinyimkuu amesema amefurahishwa na namna ambavyo mkuu wa wilaya anafanya kazi zake huku akilenga kukutana na makundi ya watu wa chini ambayo ndiyo yenye changamoto nyingi huku akimtaka asiache kushuka kusikiliza kero za makundi mengine mara baada ya kumaliza hili kundi la Mama na Baba lishe.
Sambamba na hilo Mwinyimkuu ambaye ni Baba lishe wa mtaa wa Buyuni amemuomba Mkuu wa Wilaya hiyo kuwaunganisha wafanyabiashara wa kata ya Pemba Mnazi na kuwaweka sehemu moja huku akipendekeza eneo la sokoni kujengwa vibanda watakavyotumia wafanya biashara wote huku akisisitiza kuwa kwa kufanya hivyo kutaongeza tija kwenye biashara yao ya chakula huku wafanya biashara wa mboga na matunda wakinufaika kutokana na Muingiliano utakaokuwepo.
"Ili Serikali iweze kutuhudumia sisi Baba lishe na Mama lishe ni vyema mkatukusanya na kutuweka pamoja na kama itakupendeza utujengee vibanda kwenye eneo la soko ambapo kutakua na uwezekano wa wafanya biashara wote kukaa sehemu moja na hivyo kusababiisha mzunguko wa fedha kuwa mkubwa" Alisema Shabani Mwinyimkuu.
Sambamba na hilo bi. Asha Lyimo aliwasilisha ombi la kusaidiwa upatikanaji wa mikopo ili waweze kukuza mitaji yao na kuifanya biashara ya chakula kwa weledi na ufanisi wenye matokeo chanya kwa jamii na Serikali kwa kuwawezesha kukusanya kodi husika kwa urahisi.
"Tunakuomba Mkuu wetu utusaidie kupata mikopo kwani mitaji yetu ni dhaifu na haikidhi kufanya biashara hii kwa viwango stahiki," Alisema.
Mkuu wa Wilaya hiyo Bi. Bulembo, alitumia fursa hiyo kumuagiza Mkurugenzi wa Manispaa Erasto kiwale aliyewakilishwa na Afisa Maendeleo ya Jamii Sigilinda Mdemu kufanya marekebisho ya miundo mbinu ya soko la Tundwi Center ili kuzuia maji ya mvua kujaa ndani ya soko na kusababisha uharibifu wa bidhaa za wafanya biashara katika soko hilo.
"Mkurugenzi, nikuombe utafute namna ya kuwaondolea adha wafanya biashara hawa kwa sababu mvua zipo karibu kuanza ili tusiendelee kuwapa hasara zinazosababishwa na maji ya Mvua kuvujia kwenye bidhaa zao," Alisema DC Bulembo.
Samba na hilo, Mhe. Bulembo alimtaka Afisa Maendeleo kata kuwapitia watoa huduma za chakula na kuwapa elimu ya namna bora ya kupata mikopo ya serikali ili mara baada ya mchakato wa maboresho ya mikopo itakapokamilika basi kundi hilo kwa kata ya pembamnazi liwe sehemu ya wanufaika huku akimsisitiza afisa biashara kuchukua maoni ya kutaka kuwekwa pamoja na kuyafanyia kazi.
Naye Afisa Afya Manispaa ya kigamboni Maua hayeshi alitoa elimu ya umuhimu wa kupima afya kwani sheria inawataka wafanya biashara wa chakula kupima afya na kuzingatia usafi wa mazingira katika maeneo yao ya kazi huku akiwasisitiza umuhimu wa kuvaa mavazi rasmi (sare) wakati wanapotekeleza majukumu yao.
Aidha Afisa Lishe (w) Bi. Henerietha Kyomushula amewataka kuzingatia uaandaaji wa mapishi ulio sahihi ikiwemo kutoivisha mboga za majani kupita kiasi, huku akiwataka kuzingatia matumizi madogo ya mafuta, sukari na chumvi ili kujiepusha na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo shinikizo la Damu.
Gezaulole Kata ya Somangila, Kigamboni
Anuani ya Posta: 36009 Dar es Salaam
Simu: +255222928468
Simu ya Mkononi: +255222928468
Bara pepe: info@kigambonimc.go.tz
Haki MilikiĀ©2017 Manispaa ya Kigamboni . Haki zote Zimehifadhiwa