MAANDALIZI TAMASHA LA HAMASA KWA WANANCHI KUSHIRIKI SENSA YAWIVA,MKUU WA WILAYA YA KIGAMBONI APANGA MIKAKATI KWA KUSHIRIKISHA NGAZI ZOTE ZA WILAYA
Mkakati wa Tamasha la kuhamasisha wananchi wa Wilaya ya Kigamboni kushiriki katika Sensa ya watu na makazi unaendelea vizuri ambapo leo hii 10/8/2022 Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni amekaa kikao na Viongozi mbalimbali wakiwepo na Wadau mbalimbali kwa ajili ya kujadili utekelezaji wa Tamasha hilo.
Akiongea Mh.Fatma Almas Nyangasa wakati akifungua kikao hicho amesema kuwa zoezi la Sensa ni zoezi kubwa la kitaifa ambapo serikali imefanya maandalizi makubwa kwa ajili ya kufanikisha zoezi hili ambapo kwa sasa maandalizi yapo kwenye hatua ya mwisho ya kutoa mafunzo kwa watakaoshiriki kupita nyumba kwa nyumba kuhesabu watu."Ni wajibu wetu sasa kuhamasisha wananchi wetu kushiriki kikamilifu katika zoezi hili ili liwe na ufanisi."alisema Nyangasa
Aidha ameongeza kuwa baadhi ya wananchi hawana uelewa kwa undani umuhimu wa zoezi hili hivyo kuna haja ya kuwahamasisha na kuwaelimisha kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo hii ambayo leo imetukusanya hapa ili kujadiliana kwa pamoja namna tutakavyotekeleza Tamasha hili lenye lengo la kuelimisha na kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika kuhesabiwa.
Aidha aliwapa fursa kamati ndogo kutoa mapendekezo yao ili washiriki wa kikao waweze kutoa maoni yao na kuongezea mawazo yao katika kufanikisha utekelezaji.
Tamasha hili linatarajiwa kufanyika tarehe 20 ambapo siku sita kabla ya tamasha kutakuwa na utekelezaji wa shughuli mbalimbali kwenye kata za Kigamboni zenye lengo la kuhamasisha wananchi kuelekea kilele siku ya tamasha.
Shughuli hizo zitahusisha jogging asubuhi kutoka ferry hadi Mji mwema kwa siku ya Kwanza 13/8/2022 ,tarehe 16/8/2022 uhamasishaji utafanyika Kisarawe II na Tundwi Songani,18/8/2022 uhamasishaji utafanyika Kimbiji na Dege,18/8/2022 kutakuwa na bonanza la mpira litakalofanyika viwanja vya Mji mwema,18/82022 Mkuu wa Wilaya ya kigamboni atakutana na makundi maalum ya watu wenye ulemavu katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya kigamboni,19/8/2022 Mkuu wa Wilaya atakutana na wavuvi saa 4:00 asubuhi na tarehe 20/8/2022 ndio itakuwa kilele na tamasha litafanyika katika viwanja vya mjimwema ambapo litaanza saa 5:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni.
Katika Tamasha hilo kutakuwa na upimaji wa afya ikiwepo upimaji na chanjo ya COVID na utoaji elimu ya lishe ,vilevile kutakuwa na michezo mbalimbali,wasanii watatumbuiza ,viongozi watatoa salam,fursa za wilaya ya kigamboni zitaongelewa.
Hivyo mwananchi wa kigamboni anza kujipanga kuhudhuria Tamasha hili litakalokuwa na mambo mengi yenye manufaa.
Kikao kimehudhuriwa na Mbunge wa Kigamboni Mh.Faustine Ndugulile,Katibu Tawala wa Wilaya ndg.James Mkumbo,Viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa,Kamati ya Ulinzi na usalama,viongozi wa dini,Meya wa Manispaa ya Kigamboni Mh.Ernest Mafimbo,na Madiwani,Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni ndg. Erasto Kiwale na menejimenti yake,watendaji wa Kata,Watendaji wa Mitaa,Viongozi wa kikundi cha wasanii,Mwenyekiti wa bodaboda,Mwenyekiti wa wenye malori,Mwenyekiti wa wafanyabiashara,Mwenyekiti wa wasanii. Kigamboni
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano serikalini
Gezaulole Kata ya Somangila, Kigamboni
Anuani ya Posta: 36009 Dar es Salaam
Simu: +255222928468
Simu ya Mkononi: +255222928468
Bara pepe: info@kigambonimc.go.tz
Haki MilikiĀ©2017 Manispaa ya Kigamboni . Haki zote Zimehifadhiwa