Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni leo imefanya semina ya mafunzo ya elimu ya maadili ya utumishi wa umma, uwajibikaji na mapambano dhidi ya Rushwa kwa watumishi wake kwa lengo la kuwakumbusha watumishi namna wanapaswa kuenenda lakini pia kuona wajibu waliokuwa nao kwenye mapambano dhidi ya rushwa.
Akifungua semina hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni ,katibu tawala wa wilaya Bi. Rahel Mhando amesema kuwa, ofisi ya mkuu wa Wilaya imeona ni vyema kuwakumbusha watum...ishi wake kuhusiana na suala zima la maadili na rushwa hasa katika kipindi hiki cha uadilifu kazini ili wananchi waweze kupata huduma wanayotarajia.
Akizungumzia mada ya Maadili mtoa mada kutoka chuo cha mwalimu nyerere Bw. Daniel Mafie amesema kuwa maadili ni kinga ya kwanza dhidi ya rushwa na mambo mengine maovu ambapo alieleza kuwa maadili pia lazima yaanzie kwenye ngazi ya familia ili kupata viongozi bora.
Aidha ameeleza pia maadili yoyote lazima yazingatie taaluma, uaminifu, na uwajibikaji na kueleza kuwa utumishi wa umma ni heshima hivyo watumishi wanapaswa kutenda kazi kulingana na matarajio ya wananchi kwa kuzingatia kuwa Serikali kazi yake ni kutoa huduma kwa jamii.
Kwa upande wake Afisa TAKUKURU upande wa dawati la elimu Bi.Nerry Mwakyusa amesema kuwa anaipongeza ofisi ya mkuu wa Wilaya kwa uzalendo na kutenga muda wa kupata elimu juu ya mambo ya Rushwa na kuwaomba wengine kuiga mfano huu ili mapambano ya rushwa yaweze kufanikiwa.
Aidha aliongeza kuwa mapambano dhidi ya rushwa si ya Serikali au TAKUKURU pekee bali ni ya jamii nzima kwa kutambua kwamba rushwa inasababisha kero kubwa kwa Serikali na wananchi hususani katika harakati za kujiletea maendeleo.
Aliongeza kuwa vitu vinavopolekea rushwa kuendelea kuwepo ni ubinafsi na uroho wa mali, mmomonyoko wa maadili, kanuni na taratibu zinazotoa mlolongo mrefu wa upatikanaji wa huduma, utashi mdogo na mazoea mabaya ambayo watu wanayo juu ya rushwa ambapo haya yakiondoka itasaidia kwenye mapambano dhidi ya Rushwa.
Vile vile alieleza kuwa iwapo watumishi wa umma watashiriki kikamilifu kupambana na rushwa ufanisi wa kazi na huduma za jamii utaboreshwa, wananchi watakua na imani na serikali,maendeleo ya nchi yataharakishwa, wawekezaji wengi watakuja kuwekeza na kuondoa vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu.
Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Kigamboni Bw.Phillip Joseph amesema elimu ya rushwa inaendelea kutolewa na kuwataka watumishi waliopata elimu hiyo kuelimisha jamii na kwamba isiwe wao wakawa ndio chanzo cha kulalamikiwa juu ya vitendo vya rushwa.
Semina hii imefanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya Kata ya Mjimwema na kuhudhuriwa na watumishi kutoka ofisi ya mkuu wa Wilaya na wawezeshaji kutoka TAKUKURU na Chuo cha Mwalimu Nyerere Kigamboni.
Bw. Daniel Mafie kutoka chuo cha Mwalimu Nyerere akitoa Elimu ya Maadili kwa watumishi Wa umma
Elimu ya maadili ikitolewa
Watumishi wakifatilia utolewaji Wa Elimu
Mkuu Wa TAKUKURU Wilaya ya Kigamboni Bw. Philip Joseph akizungumza kwenye mafunzo ya Rushwa na wajibu Wa watumishi Wa umma
Afisa Tawala Wilaya ya Kigamboni akishukuru wawezeshaji Wa Elimu na Katibu Tawala kwa Elimu waliyopata kama watumishi
Afisa TAKUKURU Wilaya ya Kigamboni (Dawati la elimu) Bi.Nerry Mwakyusa akitoa Elimu kwa watumishi
Watumishi pamoja na watoa Elimu wakiwa kwenye picha ya pamoja
Gezaulole Kata ya Somangila, Kigamboni
Anuani ya Posta: 36009 Dar es Salaam
Simu: +255222928468
Simu ya Mkononi: +255222928468
Bara pepe: info@kigambonimc.go.tz
Haki MilikiĀ©2017 Manispaa ya Kigamboni . Haki zote Zimehifadhiwa