Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni inatarajia kujenga Maabara,wodi ya mama na mtoto pamoja chumba cha upasuaji(Theater) katika kituo cha Afya cha Kimbiji kilichopo mtaa wa Kizito Huonjwa kata ya Kimbiji.
Ujenzi huo unatarajiwa kugharimu jumla ya shilingi milioni 400 zilizotolewa na Ofisi ya Rais TAMISEMI katika mpango wa uboreshaji wa huduma za Afya nchini.
Timu ya ukaguzi toka ofisi ya Rais-TAMISEMI ikiongozwa na ndg Mwita Weibe ilifika kituoni hapo kuona hatua iliyofikiwa ambapo mpaka sasa eneo la ujenzi limeshasafishwa tayari kwa kuanza ujenzi. Ndg Mwita alisisitiza kuwa Ofisi yake inatarajia kuona ujenzi huo unakamilika ndani ya miezi miwili kuanzia sasa ili kituo hicho kiweze kutoa huduma iliyokusudiwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ndg Renatus Mchau aliwahakikishia wajumbe hao toka Tamisemi kuwa mpaka kufikia mwezi Aprili 2018 ujenzi huo utakuwa umekamilika na kuanza kutumika. Ujenzi huo unatajiwa kusimamiwa na wataalam wa ujenzi wa manispaa kwa kuwatumia mafundi wa kawaida na pia kwa kuwashirikisha wananchi katika hatua zote za ujenzi.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kimbiji Mh.Sanya Bunaya amesema wao kama kata wamejipanga katika mitaa yote kushirikiana na mafundi katika shughuli ndogo ndogo kama kuchota maji, mchanga na kusomba matofali ili kupungiuza gharama za ujenzi na pia kwa kushirikiana na kamati ya uongozi wa kituo hicho kinachoongozwa na Mzee Ally Msumi ambao wote kwa pamoja wamekubaliana kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.
Timu hiyo ya ukaguzi pia ilitembelea hospitali ya Vijibweni ambapo baada ya kuongea na watumishi wa hospitali hiyo ilikagua pia ujenzi wa chumba cha X-ray na Utra sound kinachojengwa hospitalini hapo. Mganga mkuu wa Manispaa ya Kigamboni Dr.Charles Mkombachepa alisema ujenzi huo unatajajiwa kukamilika ndani ya miezi miwili na kuanza kutumika ili kuwapunguzia wananchi adha ya kusafiri umbali mrefu kwenda kutafuta huduma hiyo nje ya Manispaa ya Kigamboni.
Gezaulole Kata ya Somangila, Kigamboni
Anuani ya Posta: 36009 Dar es Salaam
Simu: +255222928468
Simu ya Mkononi: +255222928468
Bara pepe: info@kigambonimc.go.tz
Haki MilikiĀ©2017 Manispaa ya Kigamboni . Haki zote Zimehifadhiwa