Wataalamu kutoka Taasisi isiyokuwa ya Kiserili inayofanya shughuli za ulinzi na uhifadhi mazingira na rasilimali za maliasili (LEAT) kwa kushirikiana na watalaamu wa Manispaa Leo wamefika Manispaa ya Kigamboni Kata ya Vijibweni kwa lengo la kubaini changamoto za kimazingira na kutoa mapendekezo ya namna ya kutatua changamoto hizo.
Akizungumza na wataalamu kutoka LEAT Mara baada ya kutembelea eneo la wazi lililopo Vijibweni linalomilikiwa na mtu binafsi na kutumika kama eneo la kutupa taka Diwani wa Kata ya Vijibweni Mhe. Zakaria Mkundi amesema kuwa uharibifu unaoonekana kwenye eneo lililopo pembezoni mwa Bahari ulikuwa mkubwa lakini Manispaa imepambana kuhakikisha wananchi wanaacha kutupa taka maeneo ambayo hayajaainishwa kisheria.
Mhe. Mkundi ameongeza kwa kusema kuwa kama Manispaa imeandaa eneo maalumu litakaloruhusu wananchi kukusanya taka na kwenda kutupwa kwenye dampo la lingato lililopo Kisarawe II kwa lengo la kukabiliana na uharibifu wa mazingira.
Aidha amesema utaratibu wa usafi wa kila jumamosi umesaidia kwa kiwango kikubwa kuhamasisha wananchi kufanya usafi na kufanya mazingira yao nadhifu.
" Natoa wito kwa wananchi wa Vijibweni na wanakigamboni kwa ujumla kutunza mazingira kwa ustawi wa afya zao kwani bila Afya hatuwezi kufanya shughuli zozote za kimaendeleo'' alisema Diwani.
Afisa Mazingira wa Manispaa ya Kigamboni Hussein Mwoma amesema kuwa kama wataalamu wamebaini watu wamekuwa wakivamia maeneo na kuchimba michanga na mashimo yanayobaki kutumika Kama dampo kinyume cha taratibu hivyo kama Manispaa inajipanga kutafuta wamiliki wa maeneo ya wazi ambao hawajayaendeleza na kuweka ulinzi ili kuzuia matumizi yasiyosahihi yanayoleta athari kwa jamii.
Kwa upande wa mitaro inayoonekana kutuamisha maji, Hussein amesema taarifa itafika kwa TARURA ambao ndio wahusika wa Barbara za mitaa ili kuona namna bora itakayofanyika ili kuruhusu mitaro kuweza kufanya kazi ya kutiririsha maji kama ilivyokusudiwa.
Mtaalamu kutoka LEAT , Baraka Thomas ( wakili) amesema kuwa kama taasisi yenye lengo la kuhimiza usafi wa mazingira na kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa wao kuwa sehemu ya usafi, wapo tayari kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya mazingira ili kulinda afya na mazingira wanayoishi kwa kushirikiana katika kutatua changamoto zinazobainika kwenye maeneo yao.
LEAT imepata ufadhili kwa Shirika la Legal Service Facility kuendesha mradi kwa miaka miwili wenye jina la " kulinda hali za kimazingira kwa wanawake,vijana, wasichana na jamii kwa ujumla kupitia kuwezesha jamii katika masuala ya kisheria jijini Dar es Salaam.
Mradi huu upo katika Manispaa zote 5 za Jiji la Dar es Salaam ambapo kwa Kigamboni awamu ya kwanza utafanyika katika kata za Kigamboni na Vijibweni.
Gezaulole Kata ya Somangila, Kigamboni
Anuani ya Posta: 36009 Dar es Salaam
Simu: +255222928468
Simu ya Mkononi: +255222928468
Bara pepe: info@kigambonimc.go.tz
Haki MilikiĀ©2017 Manispaa ya Kigamboni . Haki zote Zimehifadhiwa