DC KIGAMBONI AKUTANA NA WAKUU WA IDARA NA VITENGO ,AWEKA MSISITIZO KATIKA UTENDAJI KAZI
Leo 2/2/2023 Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mh.Halima Bulembo amekutana na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Manispaa hiyo lengo likiwa kutambuana na kuelekezana masuala ya utekelezaji wa kazi.
Akianza Kwa kuwashukuru watendaji kufika katika kikao
pia amewataka Watendaji hao wa idara kuonyesha ushirikiano katika utekelezaji wa kazi hasa katika masuala ya utekelezaji wa miradi ambapo amesema hatapenda kuona udanganyifu, ufanyaji kazi wa mazoea unaopelekea miradi kutokukamilika kwa wakati hivyo atakuwa mfatiliaji kwa karibu Sana."Mh.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anatoa pesa nyingi Sana kwa ajili ya miradi nasi ni wasaidizi wake kuhakikisha miradi hiyo unaisha kwa wakati na kwa ubora hivyo tusimuangushe.
Akiongelea suala la Mapato amesema kuwa hatataka kuona mapato yanasuasua katika ukusanyaji hivyo amewataka kuwa wabunifu katika ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha mapato yanakuwa na kuongezeka .
Aidha akizungumzia suala la utatuzi wa migogoro ya ardhi ikiwa ni moja ya kipaumbele chake atakachoshughulika nacho ametaja baadhi ya migogoro hiyo ni uuzwaji wa ardhi kwa mtu zaidi ya mmoja, ucheleweshaji wa hati za viwanja, akizungumzia hilo amesema baadhi ya migogoro inasababishwa na ofisi za Manispaa na baadhi ni kutokana na wananchi ,hivyo amewataka maafisa ardhi kumpa orodha ya migogoro iliyopo na hatua zilizofikiwa katika migogoro hiyo na ambayo bado haijashughulikiwa na ambayo ipo mahakamani na hatataka kudanganywa katika hilo, lengo likiwa ni kutaka kuwasaidia wananchi na kupunguza migogoro.
Aidha katika kuwahudumia wananchi atataka kuona wananchi wanahudimiwa kwa wakati na kusaidiwa kwa wakati wakieleweshwa hivyo hatataka kuoana foleni ya wananchi katika kupata huduma kutokana na urasimu wakati huohuo kuepuka lugha mbaya.
Aidha kwa upande wa idara ya Mipango na uchumi amewata kuwasilisha taarifa za miradi katika hatua zilizofikiwa, changamoto na utekelezaji upo vipi.
Akizungumzia miradi ya Afya amemtaka mganga Mkuu kusimamia na kutumia fedha za miradi hasa ya serikali kuu kwa umakini,miradi isimamiwe na kuisha kwa wakati na kuepuka mtindo wa pesa kuisha hali ya kuwa mradi haujaisha,akiongelea kuhusu huduma za watumishi wa afya amemtaka DMO kushughulikia lugha mbaya zinazotolewa na wahudumu wa Afya kwa wananchi azungumze nao.
Kwa upande watumishi wa elimu amemtaka Afisa elimu kushughulikia haki za walimu na kuhakikisha haki zao kupatikana kwa wakati na kujipanga mikakati ya kuwamotisha walimu wanayofanya vizuri na wale wanayofanya vibaya kujua tatizo ni nini pamoja na kuwajengea uwezo,katika hili ameahidi kukaa kwa pamoja na ili kupanga mikakati kuinua elimu KGMC
Kwa upande wa TASAF amewataka kushughulikia kero na malalamiko aidha kutoa elimu kuwaelimisha hasa TASAF ni kwa ajili ya nani maana baadhi wamekuwa wakilalamika bila kujua walengwa hasa wa TASAF ni kina nani.
Katika suala la usafi amesema Kigamboni inajitajidi, katika siku chache alizokaaa lakini bado Juhudi zinahitajika katika kuhakikisha wananchi wanazingatia usafi sheria ndogo zitumike ipasavyo na kupanga mikakati kuangalia namna ya kuweza kurekebisha hali ya usafi.
Akizungumzia suala la Mwenge amesema tayari ratiba zimetoka na amewataka wahusika kuanza kujiandaa mapema kwa upande wa miradi ya maendeleo.
Akizungumzia mikopo alitaka kujua changamoto zilizopo ambapo kaimu mkurugenzi ndg.Mauna alieleza baadhi ya changamoto hasa wakati wa usajili katika mfumo ambapo vikundi vimeendelea kupewa maelekezo kuhakikisha changamoto hiyo inaondoka.
Aidha amewataka mainjinia kutoa ushauri na maelekezo ya ujenzi wa miradi mbalimbali kwa weledi ili kuepuka hasara baada ya ujenzi.
Kwa upande wa TANESCO amewataka kushughulikia changamoto zinazojitokeza kwa upande wa umeme kwa wakati kwani hii inakuwa ni kero kwa wananchi aidha ameahidi kukutana nao ,TARURA nao amewataka kushughulikia changamoto na kero zinazojitokeza kwa upande wa masuala ya barabara na kuendana na Kasi katika utatuzi wa changamoto hizo.
Mwisho DC Mh.Halima ameomba Sana ushirikiano,upendo na uwazi ili kuliendesha gurudumu la maendeleo Kigamboni.
Akitoa neno kaimu mkurugenzi ndg.Juvelnas Mauna amemshukuru DC kwa kikao hicho na pia amemhakikishia ushirikiano na Menejimenti "kama timu ya ushindi tutatoa ushirikiano wakati wote na kufanya kazi nawe kwa ukaribu na hakuna kitakachoharibika kwani Kumekuwa na ushirikiano mkubwa kati ya ofisi hizi mbili"alisema ndg.Mauna Kaimu Mkurugenzi.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI KGMC
Gezaulole Kata ya Somangila, Kigamboni
Anuani ya Posta: 36009 Dar es Salaam
Simu: +255222928468
Simu ya Mkononi: +255222928468
Bara pepe: info@kigambonimc.go.tz
Haki MilikiĀ©2017 Manispaa ya Kigamboni . Haki zote Zimehifadhiwa