Mkuu wa Wila ya Kigamboni Mh. Hashimu Mgandilwa ametoa siku 30 kwa wawekezaji ambao maeneo yao hayajaendelezwa muda mrefu kuyaendeleza kwani kinyume cha hapo sheria itachukua mkondo wake, huku akiwatoa shaka wawekezaji waliokuwa wamesitisha kuendeleza maeneo yao kwa kuhofia KDA(Kigamboni Development Agency) , na kuwaomba kuendeleza uwekezaji wao kwani KDA imefutwa.
Akizungumza ofisini kwake leo na waaandishi wa habari , Mkuu wa Wilaya amesema kuwa KDA imefutwa na shughuli zote kukasimiwa Manispaa hivyo kuwatangazia wale wote waliokuwa wanasuasua kuendeleza maeneo yao kuwa wanaruhusiwa kuendeleza kwa kufata utaratibu wa kuwa na vibali na ramani za mipango miji.
" Mnaruhusiwa kuendeleza maeneo yenu kwa kufuata utaratibu lakini pia wawekezaji waliohodhi maeneo bila kuyaendeleza nimetoa siku 30 kuendeleza maeneo yao kinyume na hapo kwa mamlaka tuliyopewa tutapendekeza wanyang'anywe na kupewa watu wenye uwezo wa kuyaendeleza"alisema Mkuu wa Wilaya
Akizungumzia ujenzi wa vibali Mkuu wa Wilaya amesema kuwa kujenga bila vibali ni kinyume cha taratibu ndio maana ameelekeza Manispaa kuhakikisha vibali vinapatikana ndani ya siku 5 tangu kuombwa ili kurahisisha upatikanaji wake na kuondoa malalamiko ya wananchi kuhusu kucheleweshewa vibali.
Kwaupande wa viwanja vilivyopo fukweni (beach plot) Amesema kuwa ni maeneo ya uwekezaji na sio maeneo ya kujenga makazi kama ambavyo wengine wamefanya na kuwataka waliojenga makazi kuona namna gani wataweza kurejesha maeneo hayo kuwa ya uwekezaji kama yalivyokusudiwa awali.
Akiongelea ujenzi wa ndani ya mita 60 Mkuu wa Wilaya amaesema kuwa ujenzi wa mita 60 huaruhusiwa sababu ni eneo la wazi hivyo kama mtu atahitaji kujenga anapaswa kufuata taratibu kwa kupata vibali maalumu na ambavyo vitamtaka kujenga majengo ambayo si ya kudumu.
Wakati huohuo Mh.Mgandilwa amewakaribisha wawekezaji kuwekeza kigamboni kwani kuna ardhi ya kutosha na asilimia 60hadi 70 imekwisha pimwa hivyo wawekezaji wa sekta zote wanakaribishwa kwani miundombinu ya umeme, barabara na maji inaimarishwa katika kuweka mazingira rafiki ya kuwekeza.
Mwisho aliwaasa wananchi kuacha kuwakaribisha wahamiaji haramu na kusema kuwa Tanzania ni sehemu salama wasiingizwe wahamiaji haramu ambao kesho na keshokutwa watakuja kuharibu taswira ya nchi.
"wahamiaji haramu sio rafiki kwa maendeleoya nchi, tuendele kuwakataa" alisema Mkuu wa Wilaya
kwa upande wake Diwani na Mwenyekiti wa Kamati ya uwekezaji Manispaa ya kigamboni Mh. Dotto Msawa amewahakikishia wawekezaji usalama na kusema kuwa ardhi ya kutosha ipo kwaajili ya uwekezaji hivyo wawe huru kuwekeza katika sekta zote.
Naye kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni Bi. Nice Mwakalinga amesema kuwa, Manispaa imejipanga kuhudumia wananchi na ipo tayari kutoa vibali ndani ya siku 5 badala ya wiki 2 zilizokuwa zinatumika hapo awali na kuwasisitiza wananchi kufuata taratibu katika kuhakikisha wanapata vibali kwa wakati.
Amesema kuwa katika kuhakikisha utekelezaji wa mipango miji Halmashauri kwa bajeti yake ya ndani imetenga bajeti kwaajili ya kutengeneza mpango mdogo utakao jumuishwa kwenye Master plan ya Mkoa wa Dar es Salaam ambao unalenga kuendeleza na kupanga mji mdogo wa Kigamboni ambapo kwa sasa upo hatua ya utekelezaji.
Mkuu wa Wilaya amezungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza ziara yake ya kukagua maeneo ya uwekezaji yaliyopo pembezoni mwa bahari wiki iliyopita ,yenye lengo la kuimarisha ulinzi na usalama, kuwatambua wamiliki wa viwanja vilivyopo fukweni(beach plots) na kuangalia miundombinu hususani ujenzi wa mita 60 kutoka usawa wa bahari.
.
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mh. Hashim Mgandilwa akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake leo
Kaimu Mkurugenzi Bi. Nice Mwakalinga akifafanua juu ya utaratibu wa utoaji wa vibali vya ujenzi alipokuwa akizungumza na waandshi wa Habari ofisini kwa Mkuu wa Wilaya.
Diwani wa Kata ya Kigamboni na Mwenyekiti wa Kamati ya uwekezaji Manispaa ya Kigamboni Mh.Dotto Msawa akikaribisha wawekezaji kuja kuwekeza Kigamboni kutokana na uwepo wa ardhi ya kutosha.
Gezaulole Kata ya Somangila, Kigamboni
Anuani ya Posta: 36009 Dar es Salaam
Simu: +255222928468
Simu ya Mkononi: +255222928468
Bara pepe: info@kigambonimc.go.tz
Haki MilikiĀ©2017 Manispaa ya Kigamboni . Haki zote Zimehifadhiwa