Mkuu wa wilaya ya Kigamboni Fatma Almas Nyangasa amewatahadharisha walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari kutoruhusu michango holela na isiyo na tija kwani mkakati wa serikali ni utoaji wa elimu bure ili kuwezesha watoto wengi kupata elimu ikiwa ni haki yao ya msingi.
DC Nyangasa amesema hayo leo hii alipopita kwenye shule mbalimbali za msingi na sekondari kukagua ni kwa kiasi gani watoto wameripoti shuleni na iwapo kulikuwa na changamoto katika siku hii ya kwanza yavkufungua shule katika mwaka 2023.
“Mhe rais ameelekeza fedha nyingi kwenye kuboresha miundombinu ya elimu Kigamboni, hivi karibuni tumepata shilingi milioni 200 kupitia kapu la mama tumejenga madarasa 10 mapya na viti ndani, yote hii ni kuwezesha watoto wetu wapate elimu bure”,
Aidha, DC Nyangasa amewataka wazazi na walezi wenye watoto wanaotakiwa kuwa shule wanaripoti shuleni haraka, vinginevyo mzazi ama mlezi atawajibika kama hakutakuwa na sababu za msingi.
Jumla ya watoto 4863 walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza Kigamboni ambapo leo siku ya kwanza kufungua shule Wanafunzi 2586 Sawa na asilimia 53.1 wameripoti.
Kwa upande wa darasa la kwanza maoteo yalikuwa kuandikisha watoto 6981 na walioripoti ni 5400 sawa na asilimia 77 huku shule ya awali maoteo yalikuwa watoto 4291 na walioripoti ni 2742 sawa na asilimia 64.
Gezaulole Kata ya Somangila, Kigamboni
Anuani ya Posta: 36009 Dar es Salaam
Simu: +255222928468
Simu ya Mkononi: +255222928468
Bara pepe: info@kigambonimc.go.tz
Haki Miliki©2017 Manispaa ya Kigamboni . Haki zote Zimehifadhiwa