Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Mhe. Halima Bulembo, amezindua rasmi vitambulisho vya kidigitali kwa wafanyabiashara ndogondogo katika hafla iliyofanyika viwanja vya Tungi Mnadani, Kigamboni. Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Mhe. Bulembo ametoa wito kwa wafanyabiashara kufanya shughuli zao katika maeneo rasmi kama Soko la Kibada ili waweze kutambulika na kupata huduma muhimu zinazolingana na shughuli zao.
Amesema kuwa serikali inatekeleza jukumu la kuwawezesha wafanyabiashara kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na maafisa wa maendeleo ya jamii, ili kuhakikisha kundi hilo linakua kiuchumi na kijamii. Mfumo huu mpya wa kidigitali unalenga kuboresha mazingira ya biashara na kuwaunganisha wafanyabiashara na fursa mbalimbali za kiuchumi.
Mwenyekiti wa Machinga Kigamboni, Bi. Farida Nurdin, ameishukuru Manispaa ya Kigamboni kwa kuwapatia eneo la kujenga ofisi ya machinga na kueleza matarajio ya kuanza ujenzi rasmi baada ya makadirio ya gharama. Aidha, Afisa Maendeleo ya Jamii, Bi. Enedy Mwanakatwe, ameeleza kuwa vitambulisho hivi vitawasaidia wafanyabiashara kutambulika, kuunganishwa na mifumo ya kibenki, na kuongeza ushirikiano na mamlaka kama TRA.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa, wafanyabiashara wanatakiwa kuwa na Namba ya NIDA, barua ya utambulisho kutoka kwa Mtendaji wa Mtaa, na kulipia Shilingi 20,000 ili kupata kitambulisho. Mfumo huu unatarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha ustawi wa wafanyabiashara ndogondogo Kigamboni.
Gezaulole Kata ya Somangila, Kigamboni
Anuani ya Posta: 36009 Dar es Salaam
Simu: +255222928468
Simu ya Mkononi: +255222928468
Bara pepe: info@kigambonimc.go.tz
Haki MilikiĀ©2017 Manispaa ya Kigamboni . Haki zote Zimehifadhiwa