Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mhe. Halima Bulembo ameendelea na ziara yake ya kutembelea mitaa kwa mitaa ambapo leo amefika katika mtaa wa Mahenge, Kibungo, Puna na Kwa Moris katika Kata ya Pembamnazi.
DC Bulembo amepiga marufuku ukataji wa miti hovyo na kwenda kuchoma mikaa kwani ni kosa kisheria na ni uharibifu wa Mazingira ambapo amesema iwapo atabainika mtu yeyote kufanya hivyo basi hatua kali kisheria zitachukuliwa juu yake.
Ni marufuku kukata miti, tunatakiwa kutunza mazingira yetu, miti yetu ya asili mnakata na kuchoma mikaa tukikukamata tutakuchukulia hatua kali za kisheria_ "
Pia DC Bulembo ametoa msisitizo kwa Afisa Biashara kuhakikisha wawekezaji wanapokuja kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali ni lazima watoe nafasi za ajira hata za muda kwa wananchi wanaoishi maeneo husika walipowekeza ili pia na wao wanufaike, Aidha amesema Mradi wowote wa Serikali unapofanyika ni lazima Vijana wa eneo hilo wapewe kipaumbele kwenye ajira za muda katika ujenzi wa mradi husika.
Kwa upande mwengine, DC Bulembo amewataka Vijana kuwa waaminifu pindi wanapopata ajira hizo za muda kutoka kwa wawekezaji mbalimbali wanaokuja kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao kwani changamoto kubwa imekuwa ni wizi wa vitendea kazi kama misumari, mbao na mifuko ya cement.
Aidha Meneja DAWASA amesema katika Bajeti inayokuja zimetengwa Km 50 za usambazaji wa mabomba ya maji na katika hizo kwa mtaa wa Kibungo zitafika Km 20 na kazi inaanza rasmi Mwezi Julai mwaka huu, Pia Meneja TANESCO amesema awamu ya pili ya mradi wa Umeme utaanza kutekelezwa Mwezi Julai kwa kufikia mitaa yote ya Pembamnazi ambayo bado haijafikiwa.
Akizungumza kuhusu migogoro ya Ardhi, Afisa Ardhi amesema Manispaa imeanza kutekeleza kwa kuchukua maeneo yote ambayo hayajaendelezwa hivyo kuyapima na kuyatoa kwa Wananchi, Aidha Halmashauri kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi itaanza mchakato wa kupima ardhi na kumilikisha Hati kwa wahusika ili kuondokana na Migogoro ya Ardhi.
Gezaulole Kata ya Somangila, Kigamboni
Anuani ya Posta: 36009 Dar es Salaam
Simu: +255222928468
Simu ya Mkononi: +255222928468
Bara pepe: info@kigambonimc.go.tz
Haki MilikiĀ©2017 Manispaa ya Kigamboni . Haki zote Zimehifadhiwa