Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni ni miongoni mwa Halmashauri zinazotekeleza agizo la Serikali la kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani ili kuwezesha vikundi vya wajasiriamali vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Tangu kuanzishwa kwa manispaa jumla ya bilioni 1.4 zimekwishatolewa kwenye vikundi 466 vyenye wanufaika 4390 ambapo asilimia 4 imeelekezwa kwenye vikundi vya wanawake, asilimia 4 vikundi vya Vijana na asilimia 2 vikundi vya watu wenye ulemavu.
Kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2016/17 jumla ya vikundi vya vijana 12 na 23 vya Wanawake vimepatiwa mikopo yenye thamani ya Tsh. 88,950,600, Kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2017/18 jumla ya vikundi vya vijana 76 na 19 vya Wanawake vimepatiwa mikopo yenye thamani ya Tsh. 231,394,000 na Kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 kiasi cha Milioni 500 zimetolewa kwa vikundi vya wanawake 92, walemavu 08 na Vijana 54 na bajeti ya mwaka 2019/2020 kiasi cha Tsh. milioni 616 kimetolewa kwa vikundi 182, Wanawake 126, Vijana 51 na Walemavu 5, hivyo kufanya jumla ya Bilion 1.4 kutumika kuwezesha vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu .
Utoaji huu wa mikopo ya asilimia 10 ni agizo la Serikali ambalo linaongozwa na sheria na kanuni ambazo zilitolewa mwaka 2019 zilizolenga kuwawezesha wananchi kupata mikopo isiyokuwa na riba, kutambua makundi maalumu hasa watu wenye ulemavu, wanawake na vijana kuwawezesha kujikwamua kiuchumi, kuongeza idadi ya wajasiriamali katika Wilaya na mzunguko wa fedha kwenye uchumi pamoja na Kuongeza ustawi wa jamii .
Mikopo hii imekuwa na tija kwa wakazi wa Kigamboni kwani imeweza kukuza mitaji ya wajasiriamali, imeweza kuwatoa wajasiriamali kwenye mitaji midogo waliyokuwa nayo mfano; mamalishe aliyekuwa na mtaji wa laki 3 kupitia mfuko huu umemuwezesha kuwa na mtaji wa milioni 3.
Aidha mikopo hii imewezesha kukuza pato la Taifa sababu wajasiliamali wanachangia pato la taifa kwani kuna vikundi vyenye miradi mikubwa ambavyo vinalipia kodi TRA na vina Leseni.
Kwa wajasiriamali wadogo ambao mitaji yao ni chini ya milioni 4 wanahamasishwa kuchukua vitambulisho vya ujasirimali vinavyowasaidia kufanya kazi zao kwa utulivu.
Mikopo hii pia imesaidia kutoa fursa za ajira kwa vijana hususani kipindi hiki ambacho vyuo vinazalisha wasomi wengi na kuna upungufu wa ajira rasmi, kupitia mikopo hii vijana wengi wameweza kujiunga kwenye vikundi na kuanzisha miradi na kupata mikopo inayowasaidia kujiendeleza kiuchumi.
Wimbi la uhalifu na vitendo vya ukabaji, uvutaji bangi, kukaa vijiweni bila kazi limepungua hali iliyopelekea kuwa na utulivu katika mji wa kigamboni kwani vijana hao wamejiunga kwenye vikundi, wanafanya kazi zinazowapatia vipato halali.
Kwa upande wa watu wenye ulemavu mikopo hii imewasaidia kuondoa ile hali ya utegemezi na kuombaomba kwani wamejiunga kwenye vikundi wanafanya shughuli zoa za kiuchumi zinazowawezesha kujitegemea.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Kigamboni BI. Happy Luteganya amesema kwamba wataalamu wa maendeleo wapo kuanzia ngazi ya Kata ambapo elimu ya uandaaji wa vikundi namna ya miradi yenye tija inatolewa kwa wanavikundi kabla ya kupewa mikopo.
Aidha amesema kuwa mchakato wa vikundi unaanzia ngazi ya Mtaa, Kata na hatimaye Wilaya ili kuwawezesha wataalamu kukagua ubora wa miradi yao kabla ya kupewa mikopo, ikiwa ni pamoja na kuwapa elimu ya mafunzo ya ujasiriamali kwa vikundi vyote vilivyokidhi sifa, namna ya kutunza kumbukumbu, usimamizi wa miradi na utafutaji wa masoko.
Afisa maendeleo ameendelea kwa kusema baada ya kupewa mikopo vikundi hivi vinakuwa kwenye usimamizi wa karibu ili kuona mikopo waliyopewa inaenda kutumika kwenye miradi waliyoomba na kuleta tija.
TARATIBU ZA KUPATA MKOPO WA MANISPAA.
1.Mikopo haitolewi kwa watu binafsi.
2.Vikundi vinatakiwa kuwa na katiba na watu kuanzia 10
3.Vikundi lazima visajiliwe Manispaa na Manispaa ndiyo inayosajili vikundi vyote.
4.Vikundi lazima viwe na akaunti namba na lazima isome jina la kikundi.
5.Wajumbe wa kikundi lazima wawe ni wakazi wa Manispaa husika na wawe na mradi au wazo la kuanzisha mradi.
6.Kwa upande wa Vijana umri ni kuanzia miaka 18-35 ndiyo wanaruhusiwa kukopeshwa.
7.Kwa upande wa watu wenye ulemavu lazima wawe ni watu wenye ulemavu na idadi kwa kikundi kimoja isipungue watu 5 na isizidi watu 10.
Mbali na changamoto ya urejeshaji wa mikopo kwa baadhi ya vikundi hususani vya vijana na watu wenye ulemavu Afisa Maendeleo ya Jamii bado anahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kuunda vikundi vitakavyowawezesha kupata mikopo isiyo na riba ili kuepukana na mikopo mingine yenye riba kubwa zinazowafunga kwenye kutimiza maelngo yao.
Wanachi wakiwa kwenye kongamano la utoaji wa mikopo lililofanyika novemba 209 kwenye ukumbi wa kibada garden
wanavikundi vya wananwake wkionesha baadhi ya bidhaa walizotengeneza baada ya kupatiwa mikopo.
baadhi ya wakinamama na bidhaa zao wakiwa kwenye kongamano la uwezeshaji wananchi kiuchumi
mifugo ya kikundi cha vijana
kikundi cha kinamama wachomeleaji wa samani mbalimbali wakiwa eneo lao la uzalishaji kama vitanda, bembea za watoto, madirisha baada ya kuwezeshwa na mkopo wa manispaa
Mmoja wa kijana kutoka kwenye kikundi cha vijana akipokea hundi ya fedha kutoka kwa mkuu wa Wilaya Mhe. Sara Msafiri kwaajili ya kuwezesha shughuli zao wakati wa hafla fupi ya utoaji mikopo uliofanyika Septemba 2019 viwanja vya mjimwema.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Bi. Happy Luteganya akiwa anatekeleza majukumu yake ofisini kwake.
Gezaulole Kata ya Somangila, Kigamboni
Anuani ya Posta: 36009 Dar es Salaam
Simu: +255222928468
Simu ya Mkononi: +255222928468
Bara pepe: info@kigambonimc.go.tz
Haki MilikiĀ©2017 Manispaa ya Kigamboni . Haki zote Zimehifadhiwa